Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Emily Mwakilembe, amesema kuwa matukio yanayomhusu aliyekuwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dr. Emmanuel Nchimbi, yameibua maswali mengi kuhusu mwelekeo wa siasa nchini.
Akizungumza kuhusu hatua ya Dr. Nchimbi kuacha wadhifa wake, Mwakilembe amesema kauli yake kwamba anaondoka ili kupisha mabadiliko anayoyataka Rais imemfanya atafakari kuhusu aina ya mabadiliko yanayozungumziwa.
“Dr. Emmanuel Nchimbi alisema anaacha wadhifa ule ili kupisha mabadiliko anayoyataka Mheshimiwa Rais. Nikajiuliza, toka lini Dr. Nchimbi akaogopa au hataki mabadiliko? Bado swali likaja, je, ni mabadiliko gani haya? Ni mema au mabaya? Kama ni mazuri, kwa nini ayakimbie? Jibu sina,” amesema Mwakilembe.
Mwakilembe pia amekumbusha kauli ya Dr. Nchimbi kuhusu umuhimu wa Katiba Mpya, akisema kauli yake ya kuwataka Watanzania “tupiganie Katiba Mpya” imeendelea kumfanya ajiulize kuhusu nafasi ya viongozi katika mapambano hayo.
“Nchimbi alisema, ‘Watanzania tupiganie Katiba Mpya’ Katiba hii inamfanya Rais kuwa na mamlaka makubwa sana bado tulishangaa sana; yeye ni Makamo wa Rais pia, kwa nini tupiganie wakati yeye na Rais wanapaswa kujadili na kutupa Katiba Mpya?” amesema.
Kwa mujibu wa Mwakilembe, uamuzi wa Dr. Nchimbi kutangaza kuachana na siasa nao unaongeza maswali kuhusu msimamo wake wa awali kuhusu mabadiliko ya kisiasa na Katiba Mpya.
“Kupigania Katiba Mpya ni pamoja na wewe kuwepo ndani ya mapambano hayo, sasa hili lipoje? Dr. ametupa taulo kwenye boxing stage?” amehoji.
Akihusisha matukio hayo na kumbukumbu za siasa za miaka ya nyuma, Mwakilembe amesema anapata tafakari zaidi anapokumbuka hotuba na kauli za George Simbachawene wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
“Nimekumbuka hotuba za George Simbachawene akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, zikani tafakarisha zaidi, hivi ninyi ndugu zangu mnajua ramani ya tunakoelekea? Nipeni ramani hiyo basi,” amesema.
Mwakilembe amesema taarifa za hatua za kinidhamu zinazomhusu Dr. Nchimbi, zikiwamo taarifa za kufukuzwa uanachama, zimeongeza uzito wa mjadala huo na kuibua swali la kama kiongozi huyo sasa hatakiwi tena kuwa sehemu ya siasa.
“Leo tena nasikia habari za kufukuzwa uanachama kwa Dr. Emmanuel Nchimbi, inamaanisha huyu aliyepisha mabadiliko hatakiwi hata kuwepo mlangoni?” amehoji.
Kwa upande mwingine, Mwakilembe amegusia pia mazingira ya kisiasa ya Ruvuma, akisema eneo hilo limekuwa na uzito wake katika siasa za upinzani kutokana na historia yake ya kisiasa na nafasi ya Wangoni katika siasa za eneo hilo.
Amesema kauli na dhana ya “nyumba ya pili” nayo inaacha maswali yanayohitaji majibu, hasa katika kipindi ambacho siasa za Tanzania zinaonekana kupitia mabadiliko mbalimbali.
Kwa Mwakilembe, kinachohitajika sasa si kutoa hukumu za haraka, bali kuendelea kufuatilia matukio na kauli za viongozi ili kuelewa picha kubwa ya kinachoendelea katika uwanja wa siasa.
“Anyway, haya ya ‘nyumba ya pili’ yanatafakarisha,” amesema Mwakilembe, akisisitiza kuwa matukio yanayoendelea yanaweza kuwa sehemu ya sura mpya katika siasa za Tanzania.

0 Maoni