UHAMIAJI WATOA ELIMU YA KAMPENI YA "MJUE JIRANI YAKO" KWENYE KIKOSI CHA 516KJ KIZUMBI

Na. Mwandishi Wetu, Shinyanga

Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Shinyanga imetoa elimu ya masuala ya Uhamiaji kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaohudumu katika Kikosi Cha 516KJ Kizumbi Mkoani Shinyanga  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya “Mjue Jirani Yako.”

Elimu iliyotolewa  ililenga kuwajengea uwezo na uelewa Maafisa na Askari hao kuhusu masuala mbalimbali ya Uhamiaji, hususan wahamiaji haramu na madhara yao, uraia pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji.

Akitoa elimu hiyo, Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Elizabeth Kaka, alieleza umuhimu wa jamii kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kwa kutoa taarifa kuhusu uwepo wa wageni nchini ambao wanaweza kuwa na changamoto za uhalali wa ukaazi au uwepo wao nchini.

Zaidi ya Maafisa na Askari 100 walipata elimu hiyo, ambayo pia imelenga kuimarisha ushirikiano na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Idara ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani Shinyanga.

Aidha, Askari wanaoishi nje ya kambi walisisitizwa kuwa na jukumu la kutoa taarifa pindi wanapobaini au kukutana na hali inayozua utata kuhusu uhalali wa uwepo wa mgeni nchini Tanzania.

Katika hatua nyingine, washiriki walihimizwa kutumia fursa ya kufika katika Ofisi za Uhamiaji kwa ajili ya kupata huduma za Kiuhamiaji ikiwemo maombi ya hati za safari.

Kampeni ya “Mjue Jirani Yako” inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya Uhamiaji na kuhamasisha ushirikiano katika kudhibiti uhamiaji usio halali.

0 Maoni