Na. Mwandishi Wetu
Dar es Salaam: Mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, Profesa Chotara Mweusi Sultan, amewataka Watanzania kupinga chuki zinazojengwa kwa misingi ya ukanda, kabila, dini au mahali mtu alikozaliwa, akisema misingi hiyo inaweza kuhatarisha umoja na amani ya taifa.
Profesa Sultan amesema wachambuzi na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya kauli zinazoweza kuchochea mgawanyiko katika jamii.
Akizungumzia madai yanayosambazwa kuhusu asili ya Mheshimiwa Ndejembi, amesema taarifa hizo hazipaswi kutumiwa kama silaha ya kuchochea chuki za kikanda, akisisitiza kuwa mjadala wa kisiasa unapaswa kujengwa katika hoja na si asili ya mtu.
“Kuna machapisho yanayosambazwa sana yakidai kwamba Mheshimiwa Ndejembi ni Mzanzibari, kwa mtazamo wangu, madai haya hayapaswi kutumiwa kama silaha ya kuanzisha au kuchochea chuki za kikanda,” amesema Profesa Sultan.
Amesema kwa taarifa alizonazo, Ndejembi anatoka Dodoma, huku akieleza kuwa familia yao inafahamika katika eneo hilo, hata hivyo, amesema jambo la msingi zaidi ni kwamba hata kama mtu anatoka Zanzibar, Bara au sehemu nyingine yoyote ya Tanzania, hilo halipaswi kuwa sababu ya kumchukia au kumdhalilisha.
“Hata kama mtu angekuwa Mzanzibari, uraia au asili ya mtu wa Tanzania isiwe sababu ya kumchukia au kumdhalilisha,” amesema.
Profesa Sultan amekumbusha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka utaratibu wa uwakilishi wa pande mbili za Muungano katika uongozi wa juu, akitaja Ibara ya 47 inayohusu nafasi ya Makamu wa Rais.
Amesema Watanzania wanapaswa kuacha kujenga siasa zinazowagawa kwa misingi ya “huyu ni wa Bara”, “huyu ni wa Zanzibar” au “huyu ni wa kabila fulani”, badala yake wajikite katika hoja, sera na utendaji wa viongozi.
Akisisitiza madhara ya chuki, Profesa Sultan ametaja mifano ya nchi mbalimbali za Afrika zilizopitia migogoro mikubwa, ikiwamo Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Sierra Leone na Kenya, akisema historia hizo zinapaswa kuwa fundisho kwa Tanzania.
“Chuki ikiachwa ikue inaweza kumfanya mtu amuone mwenzake si binadamu mwenzake, bali adui anayestahili kuangamizwa. Historia ya Afrika imetufundisha somo hili kwa gharama kubwa,” amesema.
Amesema maneno ya chuki yanaweza kuanza kama chapisho la Facebook, mzaha au propaganda ya kisiasa, lakini yakiachwa kukua yanaweza kugeuka kuwa ubaguzi, uhasama, vurugu na hatimaye umwagaji damu.
Profesa Sultan amewataka Watanzania kujadili hoja kwa hoja, kuwakosoa viongozi kwa kazi zao na kupinga sera wanazoona hazifai, bila kugeuza chuki kuwa msingi wa siasa.
“Tusimchukie Mtanzania kwa sababu anatoka wapi, dini yake, kabila lake au upande wa Muungano anaotoka. Tanzania ni yetu sote,” amesema.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kulinda umoja wa taifa, akisema siasa zinaweza kuwagawa watu kwa muda, lakini taifa likivunjika madhara yake yatawapata Watanzania wote.
“Usichochee chuki leo ukifikiri haitakuwa na madhara kesho. Siku chuki inapokuwa kawaida, hakuna anayejua ni nani atakuwa mwathirika wake kesho,” amesema Profesa Sultan.
“Tanzania ni yetu sote. Tujadili tofauti zetu kwa hoja, lakini tusifanye chuki kuwa msingi wa siasa zetu.”

0 Maoni