Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Maabara Kuu ya Kilimo ya Taifa (National Laboratory Centre) mkoani Dodoma, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha tija, ubunifu na utafiti katika sekta ya kilimo.
Mradi huo wa kimkakati uliozinduliwa siku ya Ijumaa Agosti 08, 2025 kama sehemu ya maadhimisho ya Nanenane umebuniwa kwa lengo la kusaidia wakulima kupata suluhisho la kitaalamu kwa changamoto mbalimbali zinazokabili uzalishaji. Kupitia maabara hiyo ya kisasa, kutakuwa na vitengo maalum vya uchunguzi wa mimea, magonjwa, wadudu, udongo na sumu kuvu, pamoja na maabara ya tishu kacha kwa ajili ya kuzalisha miche isiyo na magonjwa.
Vilevile, kituo hicho kitahusisha maabara za kuchunguza ubora wa mbegu na kufanyia uchambuzi wa kemikali kwenye udongo, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao kwa njia salama, endelevu na yenye ufanisi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akizungumza na Rais Samia, mradi huu ulipata ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na ndio utakaokuwa kituo cha kurejelewa na maabara zote nchini.
Uwepo wa kituo hicho nchini unatarajiwa kuchochea mageuzi ya kilimo, kuhakikisha wakulima wanapata huduma za kitaalamu ndani ya nchi, na kupunguza gharama za uchunguzi zinazotegemea maabara za nje.
0 Maoni