Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kesho Jumatatu kitakabiliwa na kesi mbili kubwa zinazotarajiwa kuvuta hisia za Watanzania na jumuiya ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya chama, kesi ya kwanza itasikilizwa katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, ambapo jaji anatarajiwa kutoa maamuzi kuhusiana na zuio lililowasilishwa pamoja na shauri linalohusisha kina Said Issa. Wakati huohuo, kesi nyingine ya Mwenyekiti wa chama hicho itatajwa katika Mahakama ya Kisutu.
Kutokana na hali hiyo, viongozi na wafuasi wa CHADEMA watalazimika kugawanyika kwenda kwenye mahakama hizo mbili kwa wakati mmoja, ili kufuatilia mwenendo wa mashauri hayo.
Chama hicho kimetoa wito kwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi mahakamani kuonesha mshikamano na kuunga mkono mapambano dhidi ya kile kinachoitwa hila na dhuluma za kisiasa.
CHADEMA kimeeleza kuwa, uamuzi na mwenendo wa kesi hizo si suala la chama pekee, bali ni kipimo cha heshima ya haki, uhuru na demokrasia nchini Tanzania.
0 Maoni