CHADEMA kwa sasa kipo kwenye kona ya kufa au kupona. Baada ya uchaguzi wa ndani Januari 2025, Tundu Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya akimshinda Freeman Mbowe aliyekuwa amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 20. Uchaguzi huo uliacha mpasuko mkubwa ndani ya chama.
Lissu alipoingia madarakani alitangaza msimamo wa “No Reform, No Election” akisisitiza bila mabadiliko ya kisheria na kidemokrasia, uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 usingefanyika. Kauli hiyo ilileta mgawanyiko mkubwa na kuzaliwa kundi la G55 lililopinga msimamo huo na hatimaye wengi wao wakakimbilia chama cha CHAUMA. Wakati huo mwenyekiti wa zamani alibaki kimya licha ya kuwa bado ni mjumbe wa Kamati Kuu kwa mujibu wa katiba.
Mambo yalizidi kuwa mabaya baada ya Lissu kukamatwa Aprili 2025 na kufunguliwa mashtaka ya uhaini na uchochezi. Kwa zaidi ya siku 100 sasa amekuwa rumande huku kesi yake ikisogezwa mara kadhaa na mahakama kupiga marufuku matangazo ya moja kwa moja ya mwenendo wa kesi. Viongozi wengine wa CHADEMA pia wamekamatwa na wengine kuripotiwa kupotea wakiwa njiani kumshuhudia mwenyekiti wao kizimbani.
Juni 2025, Mahakama Kuu iliamuru kusimamishwa kwa shughuli zote za kisiasa za CHADEMA na kufungia mali za chama kutokana na mgogoro wa ndani kuhusu umiliki wa mali. Hatua hiyo imezidi kukidhoofisha chama.
Pigo kubwa zaidi lilikuja pale Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokiondoa CHADEMA kushiriki uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 kwa madai ya kutokidhi masharti ya usajili wa maadili. Uamuzi huo unamaanisha chama kitapoteza nafasi hadi uchaguzi mkuu wa 2030.
Kwa sasa, mwenyekiti yupo mahabusu, chama kimesimamishwa, na haki ya kushiriki uchaguzi imefutwa. Hali hii imewaacha wanachama na wafuasi wakijiuliza swali kubwa: Je, CHADEMA kimefika mwisho wake au kitaibuka upya kutoka kwenye dhoruba hii?
0 Maoni