Banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) limeendelea kuvutia maelfu ya wananchi katika Maonyesho ya Nanenane ya Kanda ya Pwani yanayofanyika kwenye Viwanja vya Nanenane mkoani Morogoro, yakilenga kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Maonyesho hayo ambayo yalianza rasmi Agosti 2, 2025, yamekuwa jukwaa la kuonesha shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na TFS, ikiwa ni pamoja na huduma za upandaji miti, ufugaji nyuki, utalii wa misitu, usindikaji wa mazao ya misitu, pamoja na elimu ya uhifadhi wa mazingira.
Katika banda hilo, wananchi wanapata fursa ya kupatiwa elimu ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa TFS waliotoka katika mikoa mbalimbali ya Kanda ya Pwani, kuhusu njia bora za kutumia rasilimali za misitu kwa tija, bila kuathiri uendelevu wa mazingira.
Miongoni mwa huduma zinazoonyeshwa ni miche ya miti ya aina mbalimbali, mbegu bora za matunda, bidhaa za nyuki kama asali na nta, vinyago vya kitamaduni, samani na mbao zilizotengenezwa kwa malighafi ya miti kutoka katika mashamba ya miti yanayosimamiwa na TFS.
Mashamba darasa ya nyuki yaliyowekwa ndani ya banda hilo yamevutia wananchi wengi, hususan vijana na wakulima wanaotafuta njia mbadala za kuongeza kipato kupitia shughuli rafiki kwa mazingira.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wakulima kutoka Kisaki, Bi. Zena Ally alisema “Nimevutiwa sana na elimu ya ufugaji nyuki. Nimejifunza kuwa si lazima uwe na eneo kubwa kuanza, na nyuki hawaathiri mazingira kama mifugo mingine.”
Uzinduzi rasmi wa maonesho hayo kwa Kanda ya Pwani ulifanyika tarehe 2 Agosti 2025, ukiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Pinda. Akihutubia washiriki wa maonyesho, Mheshimiwa Pinda aliipongeza TFS kwa kuonesha ubunifu na utoaji wa elimu ya vitendo kwa jamii kuhusu fursa zinazopatikana katika sekta ya misitu.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira kwa mustakabali wa vizazi vijavyo na akatoa wito kwa wananchi kuchagua viongozi watakaoweka kipaumbele kwenye maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo, uvuvi na uhifadhi wa mazingira.
Maonyesho ya Nanenane yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 8 Agosti 2025. TFS itaendelea kutoa elimu na huduma katika banda lake kwa siku zote za maonesho, huku ikihamasisha jamii kutambua misitu kama msingi wa uchumi wa kijani, usalama wa chakula na mabadiliko ya tabianchi.
0 Maoni