SABABU YA AFISA MTENDAJI KUJIUA KWA SUMU YA PANYA HII HAPA

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ulowa Namba Moja, Kata ya Ulowa, Wilaya ya Ushetu, mkoani Shinyanga, Juliana Mkumbo (35), amefariki dunia katika mazingira yanayodaiwa kuwa ni ya kujitoa uhai kwa kunywa sumu ya panya.

Mwili wa marehemu ulikutwa ndani ya chumba alichokuwa amepanga, huku milango ikiwa imefungwa kwa ndani, hali iliyozua taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Tukio hilo liligundulika usiku wa Julai 16, 2025, baada ya watumishi wenzake kushindwa kuwasiliana naye kwa siku mbili mfululizo. Walipokuwa wakijaribu kumpigia simu, ilionekana inatumika muda wote, hata walipobadilisha namba hali hiyo iliendelea – jambo lililowatia hofu na kuamua kutoa taarifa kwa polisi.

Mmoja wa wakazi wa Ulowa aliyewahi kuwa kiongozi wa eneo hilo (ambaye hakupenda jina lake litajwe), alisema kuwa baada ya kutoa taarifa polisi walifika, walivunja mlango na kumkuta marehemu akiwa amelala kitandani huku mwili wake ukionyesha dalili za kutapika.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, baada ya kufika katika nyumba aliyokuwa akiishi mtendaji huyo, polisi walilazimika kuvunja mlango ambao ulikuwa umefungwa kwa ndani. Ndani walimkuta Juliana akiwa amefariki dunia juu ya kitanda chake na kulikuwa na matapishi, jambo lililowapa mashaka kuhusu chanzo cha kifo chake.

"Baada ya uchunguzi wa awali uliofanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, taarifa za daktari zinaonesha kuwa kuna dalili za matumizi ya sumu ya panya," alisema Kamanda Magomi.

Aidha, Kamanda huyo alitoa wito kwa jamii, hususan wazazi na walezi, kuwalea watoto wao katika maadili mema na kuwaandaa kisaikolojia kukabiliana na changamoto za maisha. Alisema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza matukio ya watu kujitoa uhai ambayo huacha majonzi makubwa kwa familia na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kangeme, Mlangani Mwele, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa marehemu alikuwa akiishi kijijini hapo ingawa alikuwa mtendaji wa kijiji jirani. Alieleza kuwa mwili wa marehemu ulichukuliwa saa nane usiku na kupelekwa Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

#DaimanewsUpdate

0 Maoni