MCHAKATO DIRA YA TAIFA YALETA USHIRIKIANO

Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo mchakato wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umeendeshwa. 

Akizungumza jijini Dodoma leo Julai 17, 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa Dira hiyo Dkt. Kikwete amebainisha kuwa Serikali ya Rais Samia imeonyesha ushirikiano wa kutosha, na hata wao viongozi wastaafu wameshirikishwa kutoa maoni yao.

“Mheshimiwa Rais, napenda kutoa pongezi zetu za dhati kwako kwa jinsi mchakato wa kutayarisha Dira ya 2050 ulivyoendeshwa. Ulifanyika kwa weledi wa hali ya juu, ulikuwa shirikishi na jumuishi kweli kweli. Hata sisi viongozi wastaafu tulishiriki kutoa maoni yetu kama walivyoshiriki wananchi wengine kutoa maoni yao,” amesema Dkt. Kikwete.

Ameongeza kuwa alifanikiwa kukutana na wawakilishi wa Tume ya Taifa ya Mipango mara mbili, na moja ya mikutano hiyo ilikuwa na timu iliyoongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo, marehemu Laurence Mafuru.

Aidha, Dkt. Kikwete amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaakisi mahitaji, matarajio, matamanio na maono ya Watanzania walio wengi.

Ameeleza kufurahishwa kwake kuona shabaha ya msingi ya Dira 2050 itakuwa ni kuitoa Tanzania kutoka nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini hadi kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu ifikapo mwaka 2050.

0 Maoni