Muandaaji wa mbio za NBC Dodoma Marathon, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) leo imekabidhi jezi na vifaa vitakavyotumiwa na washiriki wa mbio hizo kwa mdhamini mkuu wa mbio hizo, Kampuni ya GSM Group.
GSM Group kupitia kampuni yake tanzu ya GSM Beverages inadhamini huduma ya maji na vinywaji baridi na pia kupitia taasisi yake ya GSM Foundation ni wafadhili muhimu katika agenda tatu ya mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Julai 27, mwaka huu jijini Dodoma.
Ajenda hizo ni kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, kupanua ufadhili wa wakunga hadi kufikia wakunga 200 pamoja na kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 kwa ajili ya watoto wenye changamoto za usonji (autism) nchini.
Wakiwa Makao Makuu ya GSM Group jijini Dar es Salaam, maofisa wa NBC wamepokelewa na maofisa waandamizi wa GSM wakiongozwa na mkurugenzi wao, Gharib Said Mohamed (GSM) pamoja na mkurugenzi wa uwekezaji wa kampuni hiyo, Mhandisi Hersi Said.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Rayson Foya Foya ameishukuru GSM Group kwa kuwa mdhamini muhimu wa mbio hizo na hivyo kuwa sehemu ya harakati hizo ambazo kwa msimu huu zinalenga kukusanya fedha kiasi cha Tsh milioni 700 zitakazosaidia kufanikisha agenda hizo tatu.
Kwa upande wake Hersi Said, pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa ushirikiano huo na jitihada zake katika kukuza sekta ya michezo nchini pamoja na kuokoa maisha ya wana jamii, amesema ushirikiano huo unathibitisha jitihada na azma ya pamoja baina ya taasisi hizo mbili katika kukuza afya ya mama na ustawi wa jumla wa jamii.
"GSM Group tunaamini kwa dhati kuwa juhudi za pamoja ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazokabili jamii zetu.
Hivyo tunawakaribisha washiriki wengi zaidi kwa kuwa pia tumejipanga kuhakikisha tunakidhi mahitaji yao ya maji na vinywaji vingine baridi,’’ amesema.
Akizungumzia maandalizi ya mbio hizo, Bi Tatiana Masimba amesema mwitikio wa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi ni mkubwa huku usajili wa mbio hizi ukiendelea kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz
#NBCDodomaMarathon #NBCMarathon #NBCBank
0 Maoni