Waziri Chami Atoa Tamko la Serikali Kuhusu Ongezeko la Bei ya Sukari Nchini
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Cyril Chami (Kushoto)na Naibu wake Mhe.Lazaro Nyalandu (Kulia) katika mkutano na waandishi wa Habari ambapo Mhe.Waziri alitoa tamko la serikali kuhusu hali ya Sukari nchini.
------
1.0 Katika siku za hivi karibuni, bei ya sukari imekuwa ikipanda kwa kasi katika baadhi ya maeneo nchini na hivyo kusababisha wasiwasi mkubwa kwa Wananchi. Katika maeneo mengine, sukari hiyo hata kupatikana haipatikani kwa kiasi cha kutosha, hivyo kuifanya bei ya sukari kidogo iliyopo izidi kupaa. Bei hizo zimekuwa zikiongezeka hadi kufikia wastani wa Shilingi 2,200 kwa kilo katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.
2.0 Kutokana na hali hii, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekutana na wadau wote wa bidhaa ya sukari ili kulipatia tatizo hili ufumbuzi. Wadau hawa ni viongozi wa juu wa wizara na taasisi zinazosimamia uzalishaji na usambazaji wa sukari, wazalishaji wa sukari na wasambazaji wakuu wa bidhaa ya sukari nchini.
3.0 Katika mkutano huo, mambo yafuatayo yamebainika:
-Bei ya sukari duniani imepanda sana mwaka huu. Kwa upande wa viwanda vya Tanzania, viwanda hufungwa kati ya miezi ya Februari hadi Mei kila mwaka kwani sio msimu wa kuvuna miwa. Wenye viwanda hutumia fursa hiyo kuikarabati mitambo yao wakisubiri msimu wa uzalishaji unaoanza mwezi Juni.
Mambo haya mawili, la bei ya sukari kupanda katika soko la dunia na la sukari kutokuzalishwa kipindi hiki, yamesababisha wasiwasi wa wafanyabiashara wa sukari kuwa kungekuwepo na upungufu mkubwa wa sukari nchini kuliko ule uliozoeleka katika kipindi hiki.
Kwa vile mahitaji ya bidhaa yoyote ya kawaida yakizidi upatikanaji wake bidhaa ile hupanda bei, ni jambo la kawaida kwa wanaoiuza bidhaa ile kuwa na nia ya kuihodhi bidhaa husika,ili bei ikipanda zaidi siku za usoni wanufaike zaidi.
Hali hii inajulikana kama speculation kwa lugha ya Uchumi. Ni jambo la kawaida pia kwa baadhi ya wazalishaji na wasambazaji kuihodhi bidhaa husika kwa minajili ya kujilinda, isije ikawaishia wakati washindani wao wakingali wanayo, kwani hilo likitokea, washindani wao watanufaika na bei kubwa na hivyo kuwaondoa katika uzalishaji au usambazaji.
Tabia hii ya kujilinda inaitwa hedging against competition kwa lugha ya Kiuchumi.Hivyo hivyo hapa Tanzania,nguvu hizi mbili,speculation na hedging against competition, zimewafanya baadhi ya wenye viwanda na baadhi ya wasambazaji kuweka sukari nyingi katika maghala.
-Hata hivyo, baada ya kikao cha Mheshimiwa Waziri Mkuu na wadau wahusika kupata takwimu zote, imebainika kuwa kiasi cha sukari iliyopo nchini kinatosheleza mahitaji ya nchi kwa zaidi ya miezi miwili, yaani kuanzia sasa hadi mwishoni mwa mwezi Aprili 2011.

0 Maoni